John 9

Isa Amponya Mtu Aliyezaliwa Kipofu

1 aIsa alipokuwa akipita, akamwona mtu aliyekuwa kipofu tangu kuzaliwa. 2 bWanafunzi wake wakamuuliza, “Rabi, ni nani aliyetenda dhambi, ni huyu mtu au wazazi wake hata azaliwe kipofu?”

3 cIsa akawajibu, “Huyu mtu wala wazazi wake hawakutenda dhambi. Alizaliwa kipofu ili kazi za Mungu zidhihirishwe katika maisha yake. 4 dYanipasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenituma wakati bado ni mchana, kwa kuwa usiku waja ambapo hakuna mtu awezaye kufanya kazi. 5 eWakati niko ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu.”

6 fBaada ya kusema haya, akatema mate ardhini, akatengeneza tope kwa mate na kumpaka yule mtu kipofu machoni. 7 gKisha akamwambia, “Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu.” (Siloamu, maana yake ni aliyetumwa.) Ndipo yule kipofu akaenda, akanawa, naye akarudi akiwa anaona.

8 hMajirani zake na wale wote waliokuwa wamemwona hapo awali akiombaomba wakaanza kuuliza, “Je, huyu si yule aliyekuwa akiketi akiombaomba?” 9Wengine wakasema, “Ndiye.”

Wengine wakasema, “Siye, bali wamefanana.”

Lakini yeye akawaambia, “Mimi ndiye.”

10Wakamuuliza, “Basi macho yako yalifumbuliwaje?”

11 iYeye akawajibu, “Yule mtu aitwaye Isa alitengeneza tope, akanipaka machoni mwangu, naye akaniambia nenda ukanawe katika Bwawa la Siloamu, ndipo nikanawa nami nikapata kuona!”

12Wale wakamuuliza, “Yeye huyo mtu yuko wapi?”

Akawajibu, “Sijui.”

Mafarisayo Wachunguza Kuponywa Kwa Kipofu

13Wakamleta kwa Mafarisayo yule mtu aliyekuwa kipofu hapo awali. 14 jBasi siku hiyo Isa alipotengeneza tope na kuyafungua macho ya huyo mtu ilikuwa Sabato. 15Mafarisayo nao wakaanza kumuuliza alivyopata kuponywa. Naye akawaambia, “Alinipaka tope kwenye macho yangu, nikanawa na sasa ninaona.”

16 kBaadhi ya Mafarisayo wakasema, “Huyu mtu hatoki kwa Mungu, kwa sababu hashiki Sabato.”

Lakini wengine wakasema, “Awezaje mtu mwenye dhambi kufanya miujiza kama hii?” Wakagawanyika.

17 lHivyo wakamwambia tena yule mtu aliyekuwa kipofu, “Wewe ndiwe uliyefumbuliwa macho, wasemaje kuhusu mtu huyo?” Maana macho yako ndiyo yaliyofumbuliwa.

Yeye akawajibu, “Yeye ni nabii.”

18 mWale Wayahudi hawakuamini ya kuwa mtu huyo alikuwa kipofu, akapata kuona, mpaka walipowaita wazazi wake. 19Wakawauliza, “Je, huyu ni mtoto wenu, ambaye mnasema alizaliwa kipofu? Imekuwaje basi sasa anaona?”

20Wazazi wake wakajibu, “Tunajua ya kuwa huyu ni mtoto wetu na ya kuwa alizaliwa kipofu. 21Lakini sisi hatujui ni kwa jinsi gani kwamba sasa anaona, wala hatujui ni nani aliyemfungua macho yake. Muulizeni, yeye ni mtu mzima na anaweza kujieleza mwenyewe.” 22 nWazazi wake walisema hivi kwa sababu waliwaogopa Wayahudi kwani walikuwa wamekubaliana kuwa mtu yeyote atakayemkiri Isa kuwa ndiye Al-Masihi
Al-Masihi maana yake ni Masiya , yaani Aliyetiwa mafuta.
atafukuzwa kutoka sinagogi.
23 pKwa hiyo wazazi wake wakasema, “Yeye ni mtu mzima. Muulizeni.”

24 qHivyo kwa mara ya pili wakamwita yule aliyekuwa kipofu, nao wakamwambia, “Mpe Mungu utukufu! Sisi tunafahamu kuwa mtu huyu aliyekuponya ni mwenye dhambi.”

25Akawajibu, “Mimi sijui kama yeye ni mwenye dhambi. Lakini jambo moja ninalojua, nilikuwa kipofu na sasa ninaona.”

26Wakamuuliza, “Alikufanyia nini? Aliyafumbuaje macho yako?”

27 rAkawajibu, “Tayari nimekwisha kuwaambia, nanyi hamtaki kunisikiliza. Mbona mnataka kusikia tena? Je, ninyi nanyi mnataka kuwa wanafunzi wake?”

28 sNdipo wakamtukana na kusema, “Wewe ndiwe mwanafunzi wake, Sisi ni wanafunzi wa Musa. 29 tTunajua kwamba Mungu alisema na Musa, lakini kwa habari ya mtu huyu hatujui atokako.”

30 uYule mtu akawajibu, “Hili ni jambo la ajabu! Hamjui anakotoka, naye amenifungua macho yangu! 31 vTunajua ya kuwa Mungu hawasikilizi wenye dhambi, lakini huwasikiliza wote wanaomcha na kumtii. 32Tangu zamani hatujasikia kwamba mtu amemponya yeyote aliyezaliwa kipofu. 33 wKama huyu mtu hakutoka kwa Mungu, asingeweza kufanya lolote.”

34 xWao wakamjibu, “Wewe ulizaliwa katika dhambi kabisa, nawe unajaribu kutufundisha?” Wakamfukuza atoke nje.

Upofu Wa Kiroho

35 yIsa aliposikia kuwa wamemfukuzia nje yule mtu aliyemfumbua macho, alimkuta akamuuliza, “Je, unamwamini Mwana wa Adamu?”

36 zYule mtu akamjibu, “Yeye ni nani, Bwana? Niambie ili nipate kumwamini.”

37 aaIsa akamjibu, “Umekwisha kumwona, naye anayezungumza nawe, ndiye.”

38 abYule mtu akasema, “Bwana, naamini.” Naye akamwabudu.

39 acIsa akasema, “Nimekuja ulimwenguni humu kwa ajili ya kuhukumu, ili wale walio vipofu wapate kuona, nao wale wanaoona, wawe vipofu.”

40 adBaadhi ya Mafarisayo waliokuwa karibu naye wakamsikia na kumwambia, “Je, kweli sisi ni vipofu?”

41 aeIsa akawajibu, “Kama mngekuwa vipofu kweli, msingekuwa na hatia ya dhambi, lakini kwa kuwa mnasema, ‘Tunaona,’ basi mna hatia.
Copyright information for SwhKC